Wednesday 6 February 2013

SHULE YA SEKONDARI YA TARAKEA YAPATA MSAADA WA TSHS MILIONI 194 KUTOKA JAPAN

MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh ametoa rai kwa Watanzania kuwa waaminifu katika matumizi ya misaada inayotolewa na nchi zilizoendelea.

Utouh alisema hayo jana Dar es Salaam kwenye warsha ya kuweka saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana wa Shule ya Sekondari ya Tarakea iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa Japan nchini. Serikali ya Japan imetoa zaidi ya Sh194 milioni kwa ajili ujenzi unaotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu na kukamilika Desemba 2013.

“Ni lazima watu watambue thamani ya fedha zinazotolewa na wafadhili na wawajibike kwa matumizi sahihi ili kuwapa moyo wa kuendelea kutoa msaada katika sekta nyingine muhimu kwani kinyume na hapo ni kuwakatisha tamaa,” alisema Utouh.

Alisema kwamba kuweka saini ya ujenzi wa bweni la wasichana ni hatua ya mafanikio kwa wanafunzi wa kike wanaolazimika kutembea umbali wa kilomita nyingi hadi kufika shuleni.
“Kwa kipindi kirefu wasichana wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi hususani barabarani kutokana na kutembea umbali mrefu hadi kufika shuleni, huku wengi wakikatisha masomo yao,” alisema Utouh.

Balozi wa Japan nchini, Masaka Okada alisema, wanategemea baada ya mradi kukamilika wanafunzi wapatao 64 wataweza kuishi katika bweni hilo na kusoma katika mazingira mazuri tofauti na mwanzoni.

Alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo takriban wasichana 30 wanalazimika kukatisha masomo kila mwaka kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.
“Matumaini yangu ni kuwa mradi huu utawawezesha wanafunzi wote wa kike kumaliza masomo pasipo kukatisha kwani kumwezesha mwanamke ni jambo muhimu katika maendeleo ya nchi hii,” alisema Okada na kuongezea kuwa:

“Wanafunzi wa kike watakaokuwa wanaishi katika bweni jipya litakalojengwa watapata fursa ya kusoma kwenye mazingira mazuri na baada ya kumaliza masoma yao watakuwa chachu katika maendeleo ya nchi.”

Awali, Mkuu wa shule hiyo, Martin Kija alisema mradi huu ni mkombozi kwa wanafunzi wa kike waliokuwa wanatoka maeneo ya mbali na shule.

Kija alisema wamekuwa wakipata malalamiko kwa wasichana wanaotoka maeneo ya mbali kutokana na matatizo wanayoyapata njiani huku wengine wakilazimika kukatisha masomo yao.
(Habari hii ni kwa hisani ya Gazeti la MWANANCHI la tarehe 07/02/2013)