Monday 31 December 2012

WAOMBAJI KAZI WAMETAKIWA KUJIANDAA WANAPOENDA KWENYE USAILI

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema ofisi yake hivi sasa itakuwa ikitoa ratiba ya usaili mapema kila mara ili kuwawezesha wasailiwa kuwa na muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kwenda kwenye usaili husika.
Amesema hayo leo wakati akiongea na mwandishi wa habari ofisini kwake alipokuwa  akitoa ratiba ya usaili kwa mwezi Septemba, 2012 pamoja na tangazo la kuita kazini waombaji waliofaulu usaili uliopita. Aliongeza kuwa ili msailiwa aweze kufanya vizuri katika usaili pamoja na vigezo vya kitaaluma alivyonavyo bado anatakiwa kujiandaa vyema na kujiamini anapojibu maswali wakati anapokuwa kwenye usaili.
Daudi amesema hivi sasa dunia imekuwa ya utandawazi na fursa za ajira ni za ushindani zaidi, maana wahitimu hivi sasa ni wengi na hawana ajira hivyo ni vyema kwa wahitimu wanapoomba nafasi za kazi na kuitwa kwenye usaili wawe wamejiandaa vya kutosha ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata ajira.
Katibu, amesema kwa mwezi Oktoba, 2012 usaili utafanyika takriban katika mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo utahusisha kada zifuatazo Maafisa Tarafa daraja la II, Afisa Mtendaji wa Kata Daraja la II , Afisa Mtendaji wa Kata Daraja la III, Afisa Mtendaji wa Kijiji Daraja la II, Afisa Mtendaji wa Kijiji Daraja la III, Afisa Mtendaji Mtaa II, Afisa Mtendaji Mtaa III, Msaidizi wa Kumbukumbu Daraja la II, Mpishi Daraja la II, Afisa Utamaduni Msaidizi, Mtakwimu Msaidizi, Dereva Daraja la II, Mhudumu wa Jikoni/ Mess Daraja la II, Mlezi wa Mtoto Msaidizi, Operata wa Kompyuta Msaidizi, Msaidizi Misitu Daraja La II, Msaidizi wa Ofisi, Msaidizi Ustawi wa Jamii Daraja la II, Maendeleo ya Jamii Msaidizi Daraja la II, Mpokezi, Katibu Mahsusi Daraja la III na Mlinzi
Amesema kwa maelezo zaidi ya nafasi  hizo na wapi usaili utafanyika ni vyema waombaji wakaperuzi tovuti ya Sekretarieti ya Ajira pamoja na tovuti za Taasisi husika na kufungua tangazo la kuitwa kwenye usaili  ili kuiona ratiba nzima ya tarehe ya mchujo na usaili kama zinavyoonekana katika tangazo lenye orodha ya majina ya kuitwa kwenye usaili.
Aidha, amesisitiza ni muhimu kwa waombaji kuzingatia masharti ya tangazo pindi wanapoenda kwenye usaili kwani ni njia mojawapo ya kujua msailiwa amejiandaa kwa kiasi gani.
Wakati huohuo, Katibu amewataka waombaji wa nafasi za kazi waliofanya usaili kuanzia tarehe 7 hadi 31Agosti, 2012 katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),  Chuo cha Biashara  (CBE), Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Maji (WDMI), Chuo cha Mipango Dodoma (IRDP), Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo, COASCO, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Tume ya Mionzi (TAEC), Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI), Wakala wa Mbegu (TOSCI), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA)  kuangalia majina yao katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira pamoja na taasisi husika ili kujua waliofaulu.

Amesema kwa waliofaulu usaili wanatakiwa kuripoti kwa Mwajiri katika muda ambao umeainishwa kwenye barua zao za kupangiwa vituo vya kazi wakiwa na vyeti halisi (Originals) vya masomo kuanzia kidato cha nne na kuendelea ili vihakikiwe na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira. Aidha, barua za kuwapangia vituo vya kazi zimetumwa kupitia anuani zao za posta.

Alimalizia kwa kusema kuwa, kwa wale ambao hawataona majina yao  katika tangazo husika  watambue kuwa maombi yao hayakufanikiwa na wasisite kuendelea kuomba mara nafasi za kazi zitakapotangazwa tena.

Saturday 15 December 2012

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA UWAJIBIKAJI KATIKA SERIKALI ZA MITAA

Serikali ya Tanzania katika kuendelea kutekeleza Programu ya Uboreshaji wa Serikali za Mitaa inakusudia kuimarisha mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya Serikali za Mitaa.
Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ametumia Madaraka aliyopewa chini ya Kifungu cha 173 (C) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Kifungu cha 78 (C) cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) sura ya 288. Waziri ameziagiza Halmashauri zote Tanzania bara kuweka utaratibu wa Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo za Kata (Diwani) kuwasilisha Taarifa za Utekelezaji za Kata na kuweka utaratibu wa Wajumbe wa Halmashauri kuwauliza Wakurugenzi wa Halmashauri na Wenyeviti/Mameya wa Halmashauri Maswali ya papo kwa papo. Taarifa zitakazowasilishwa ni zile ambazo zinahusu pamoja na mambo mengine
  • Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo - ujenzi wa Madarasa, nyumba za walimu, Maabara n.k
  • Maendeleo ya Elimu - uandikishwaji watoto, utoro, ukauzi, mimba,ufundishaji n.k
  • ustawi wa jamii - majanga, magonjwa, vizazi na vifo n.k
  • shughuli za kiuchumi - upatikanaji wa wataalam, pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi n.k
  • uimarishaji wa dhana ya uzalendo na utaifa - vikundi vya vijana, mafunzo ya jeshi la Mgambo n.k
  • Taarifa za Mapokeo ya Fedha na Matumiz yake

Utaratibu huu utasaidia kutoa mwanga katika nyanja mbalimbali ikiwemo
  •  Uendeshaji wa jumla wa Halmashauri
  • Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
  • Mipango mkakati ya Halmashauri kuwaondolea wananchi umaskini
  • usimamizi na Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka husika
  • Uhifadhi wa Mazingira
  • Usalama wa Chakula, usalama wa raia na mali zao
  • Utawala bora