MWENYEKITI Mtendaji wa Kampeni za IPP Media, Regnald Mengi amejitosa
katika sakata la wasichana waliokutwa na dawa za kulevya nchini Afrika
Kusini.
Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Mengi alidai kuwa
wasichana waliokamatwa na dawa hizo wanatumika kama chambo kwani wapo
vigogo waliowatuma kufanya shughuli hiyo.
Hivi karibuni wasichana wawili raia wa Tanzania walikamatwa Afrika
Kusini wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya sh. bilioni 6.8 na
kwamba walipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es
Salaam.
Mengi alibainisha kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya inakwama
kutokana na vitendo vya rushwa. Alisema rushwa imekuwa chanzo kikubwa
cha watu kujihusisha na biashara ya dawa hizo na hivyo kuleta matatizo
kwa vijana. Alisema watu wengi ambao wanajikita katika rushwa ndiyo
wanaojiingiza katika biashara hiyo kutokana na kuwa na fedha nyingi.
Kutokana na hali hiyo, alisema wananchi wasipokuwa makini wapokea rushwa
ndiyo watakuwa watawala wa nchi.
(Nyendo Mohamed wa JAMBO LEO - www.jamboconcepts.com)