Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier
Daudi amesema ofisi yake hivi sasa itakuwa ikitoa ratiba ya usaili
mapema kila mara ili kuwawezesha wasailiwa kuwa na muda wa kutosha
kujiandaa kabla ya kwenda kwenye usaili husika.
Amesema hayo leo wakati akiongea na mwandishi wa habari ofisini kwake
alipokuwa akitoa ratiba ya usaili kwa mwezi Septemba, 2012 pamoja na
tangazo la kuita kazini waombaji waliofaulu usaili uliopita. Aliongeza
kuwa ili msailiwa aweze kufanya vizuri katika usaili pamoja na vigezo
vya kitaaluma alivyonavyo bado anatakiwa kujiandaa vyema na kujiamini
anapojibu maswali wakati anapokuwa kwenye usaili.
Daudi amesema hivi
sasa dunia imekuwa ya utandawazi na fursa za ajira ni za ushindani
zaidi, maana wahitimu hivi sasa ni wengi na hawana ajira hivyo ni vyema
kwa wahitimu wanapoomba nafasi za kazi na kuitwa kwenye usaili wawe
wamejiandaa vya kutosha ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata
ajira.
Katibu, amesema kwa mwezi Oktoba, 2012 usaili utafanyika
takriban katika mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo utahusisha kada
zifuatazo Maafisa Tarafa daraja la II, Afisa Mtendaji wa Kata Daraja la
II , Afisa Mtendaji wa Kata Daraja la III, Afisa Mtendaji wa Kijiji
Daraja la II, Afisa Mtendaji wa Kijiji Daraja la III, Afisa Mtendaji
Mtaa II, Afisa Mtendaji Mtaa III, Msaidizi wa Kumbukumbu Daraja la II,
Mpishi Daraja la II, Afisa Utamaduni Msaidizi, Mtakwimu Msaidizi, Dereva
Daraja la II, Mhudumu wa Jikoni/ Mess Daraja la II, Mlezi wa Mtoto
Msaidizi, Operata wa Kompyuta Msaidizi, Msaidizi Misitu Daraja La II,
Msaidizi wa Ofisi, Msaidizi Ustawi wa Jamii Daraja la II, Maendeleo ya
Jamii Msaidizi Daraja la II, Mpokezi, Katibu Mahsusi Daraja la III na
Mlinzi
Amesema kwa maelezo zaidi ya nafasi hizo na wapi usaili
utafanyika ni vyema waombaji wakaperuzi tovuti ya Sekretarieti ya Ajira
pamoja na tovuti za Taasisi husika na kufungua tangazo la kuitwa kwenye
usaili ili kuiona ratiba nzima ya tarehe ya mchujo na usaili kama
zinavyoonekana katika tangazo lenye orodha ya majina ya kuitwa kwenye
usaili.
Aidha, amesisitiza ni muhimu kwa waombaji kuzingatia masharti
ya tangazo pindi wanapoenda kwenye usaili kwani ni njia mojawapo ya
kujua msailiwa amejiandaa kwa kiasi gani.
Wakati huohuo, Katibu
amewataka waombaji wa nafasi za kazi waliofanya usaili kuanzia tarehe 7
hadi 31Agosti, 2012 katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Biashara (CBE), Taasisi ya
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Maji (WDMI), Chuo cha Mipango
Dodoma (IRDP), Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo, COASCO, Tume ya Vyuo
Vikuu (TCU), Tume ya Mionzi (TAEC), Taasisi ya Utafiti wa Samaki
(TAFIRI), Wakala wa Mbegu (TOSCI), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni
Bagamoyo (TASUBA) kuangalia majina yao katika tovuti ya Sekretarieti ya
Ajira pamoja na taasisi husika ili kujua waliofaulu.
Amesema kwa
waliofaulu usaili wanatakiwa kuripoti kwa Mwajiri katika muda ambao
umeainishwa kwenye barua zao za kupangiwa vituo vya kazi wakiwa na vyeti
halisi (Originals) vya masomo kuanzia kidato cha nne na kuendelea ili
vihakikiwe na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira. Aidha, barua za
kuwapangia vituo vya kazi zimetumwa kupitia anuani zao za posta.
Alimalizia
kwa kusema kuwa, kwa wale ambao hawataona majina yao katika tangazo
husika watambue kuwa maombi yao hayakufanikiwa na wasisite kuendelea
kuomba mara nafasi za kazi zitakapotangazwa tena.
No comments:
Post a Comment