Thursday, 27 February 2014

WATANO WAFARIKI KATIKA AJALI WILAYA YA HAI

Watu watano wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na gari lingine katika Barabara Kuu ya Arusha- Moshi eneo la Kia Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo juzi saa 2:00 usiku katika eneo hilo.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Sophia Christopher (18), Ashasen Emanuel (30), Amedeus Kweka (28) wakazi wa Mererani, wengine ni Adam Thegi mkazi wa Musoma na Hatib Athuman (40) mkazi wa Majengo Arusha.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, waliojeruhiwa ni Teresia John (35) Wahida Idd (28), Jerad Mtimeili (31) na Linda Mlay (22) wakazi wa Mererani Manyara.
Makunga ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, alisema gari aina ya Landrover Volkswagen lililokuwa likiendeshwa na dereva Amedeus Kweka (28) likitokea kituo cha mafuta cha Kodil liliingia barabarani huku gari ikiwaka taa moja.
Alisema dereva huyo aliingia barabarani akiwa kwenye mwendo kasi na kugongana na gari aina ya Mistubish Canter likiendeshwa na Francicy Mkongo (37) mkazi wa USA jijini Arusha na kusababisha ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robart Boaz amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasipamoja na dereva kuendesha gari likiwa halina taa wakati wa usiku.
www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment