Kama kuna eneo ambalo Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa ni
udhibiti wa usafiri wa pikipiki, maarufu kama Bodaboda. Udhaifu huo
umetoa mwanya kwa waendesha Bodaboda kuweka kando sheria za usalama
barabarani na kufanya usafiri huo kuwa janga la kitaifa kutokana na
kusababisha ajali zinazoua maelfu ya watu kila mwaka, huku maelfu ya
majeruhi wakiwa wamepoteza viungo muhimu katika miili yao.
Licha ya Jiji la Dar es Salaam kuwa machinjio
makuu ya wahanga wa ajali hizo, tatizo hilo limeikumba Tanzania Bara
kuanzia kata hadi makao makuu ya mikoa. Waendesha Bodaboda na abiria wao
wanakufa ovyo kila siku katika ajali. Serikali imebaki kuwa mtazamaji
na kujivua jukumu la kuhakikisha kwamba inalinda maisha ya raia wake.
Taarifa za Jeshi la Polisi zimethibitisha kuwapo
watu wengi wanaopoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya katika ajali
hizo, hivyo kupoteza rasilimali kubwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa
mfano, takwimu za ajali hizo mkoani Dar es Salaam zinatisha. Kamanda wa
Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga amesema watu 1,875
walikufa jijini katika kipindi cha 2011/12 kutokana na ajali za
barabarani, ikiwa ni wastani wa vifo vya watu watatu kila siku. Takwimu
za 2012/13 bado zinakusanywa, lakini jeshi hilo linasema idadi ya watu
waliokufa nchi nzima tangu mwanzoni mwa mwaka huu ni kubwa mno
ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Madaktari na
wauguzi wamesema wameelemewa na idadi kubwa ya majeruhi hao. Wengi
wamepoteza viungo muhimu, hivyo wamebaki kuwa tegemezi. Wamekata tamaa. (www.mwananchi.co.tz)
No comments:
Post a Comment