ALIYEKUWA
Waziri wa Fedha Basil Mramba, jana aliendelea kumkandamiza aliyekuwa
bosi wake na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akimhusisha moja kwa
moja na kutolewa kwa msamaha wa kodi kwa kampuni ya Alex Stewart
Government Business Assayers.
Mramba aliyaeleza hayo jana wakati
akijitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili za matumizi mabaya ya ofisi za
umma na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni na kwamba alitoa
msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo ili kutekeleza matakwa ya mkataba.
Alidai
kuwa kifungu cha 4.3.1 kilichopo kwenye mkataba huo ulioingiwa kati
ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Alex Stewart Government Business
Assayers kinasema malipo yoyote yatakayolipwa na mkataba huo
hayatotozwa kodi.
“Mimi nilichofanya ni kutekeleza matakwa ya
mkataba huu kwa sababu Waziri wa Fedha pekee ndiye mwenye mamlaka ya
kutekeleza mkataba huo,” alidai Mramba.
Mramba alikiri kuruhusu
gavana wa BoT kuilipa kampuni ya Alex Stewart, Dola za Marekani 1
milioni kama malipo ya awali, kwa ajili ya kufanya maandalizi ya ukaguzi
wa migodi ya madini, na kwamba fedha nyingine zingelipwa kwa awamu.
Mramba
alisema aliruhusu malipo hayo kufanyika kutokana na kuwapo kwa barua
ya Mei 13, 2003, kutoka kwa Katibu Mkuu wa Rais, Patrick Mombo kwenda
kwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini kuhusu mkaguzi wa dhahabu ikisema
“Rais amekubali Waziri wa Fedha na BoT watafute njia ya kuilipa kampuni
ya Alex Stewart Government Business Assayers”.
“Maagizo yote mimi
niliyachukulia kama ni ya Rais, alikuwa akiagiza watendaji wake
kutekeleza majukumu yote,”alisema Mramba na kuongeza kuwa kwa kuzingatia
makubaliano hayo alitafuta fedha hizo kupitia bungeni katika Bajeti ya
Serikali ya 2003/04.
Kuhusu mkataba, Mramba alisema kuwa
anachofahamu yeye sheria ya BoT inampa mamlaka Gavana kuingia mikataba
na kuisaini na kwamba mikataba yote aliyoingia na watu wengine ni lazima
kodi isamehewe.
Mramba aliiambia mahakama hiyo kuwa, kampuni ya
Alex Stewart Government Business Assayers ilikuwa ikitaka malipo bila
kodi na kwamba, wao walikubali kutomtoza kodi kutokana na ushauri kutoka
kwa wataalamu akiwamo gavana kuwa wamsamehe kodi vinginevyo wangemlipa
zaidi.
Hata hivyo, alisema mkataba baina ya BoT na kampuni hiyo
haukuwahi kupitia katika kikao cha Baraza la Mawaziri. “Sikudhani kama
angeweza kutiliana nao saini kwenye mkataba huo, bila Baraza la
Mawaziri kuridhia,”alisema Mramba.
Ushauri wa TRA
Mramba
alibainisha kuwa Bethar Soka ambaye alikuwa kwenye kamati iliyofanya
mchakato wa kuitafuta kampuni hiyo ya ukaguzi wa dhahabu, aliomba kupata
kauli ya TRA kama kampuni ya Alex Stewart Government Bussines Assayers
isamehewe kodi ama la, Mei 26, 2003.
Alidai kuwa baada ya Soka
kupeleka ombi hilo Mei 26, 2003, TRA katika majibu yao ya Juni 24, 2003
walisema kuwa hawapendekezi mkaguzi huyo wa dhahabu asamehewe kodi na
kwamba barua hiyo ilipelekwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wakati BoT
na kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers iliingia
mkataba Juni 14, 2003.
“Inaonyesha barua hiyo ya TRA
ilichelewa kwa siku 10, baada ya mkataba kusainiwa, hata hivyo,
ushauri huu wa TRA hatukuuhitaji hata kama ungekuja haungekuwa na
manufaa,” aliongeza kudai Mramba.
Baada ya maelezo hayo, mmoja
wa wanaosikiliza kesi hiyo, Hakimu Saul Kinemela, alimuuliza Mramba,
Wizara ya Fedha iliomba ushauri huo TRA kwa kazi gani?
Akijibu
swali hilo, Mramba alisema, "Siyo Wizara ya Fedha iliomba ushauri TRA,
bali Soka aliomba ushauri huo kama mwanakamati iliyokuwa ikifanya
mchakato wa kutafuta kampuni hiyo na kwamba Soka yeye alikuwa ni
mtumishi wa wizara yake.
Alibainisha kuwa Soka asingeweza kumshauri Waziri, anayeweza kumshauri ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu.
Mbali
na Mramba, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa
Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya
Fedha, Gray Mgonja.
Jaji John Utamwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, mwaka huu itakapoendelea na utetezi.
Utetezi wa awali
Mramba
(71) alianza kujitetea, Agosti 22, mwaka huu ambapo alidai kuwa
Serikali iliiteua BoT ifanye kazi ya kutafuta kampuni inayoweza kufanya
kazi hiyo hivyo ikaingia mkataba na kampuni iliyochaguliwa ya Alex
Stewart Government Bussines Assayers.
Waziri huyo wa zamani
aliongeza kudai kuwa aliyeagiza BOT kufanya kazi hiyo ya kumtafuta
mkaguzi wa dhahabu ni Rais wa Awamu ya Tatu, Mkapa na kwamba wakati huo
yeye akiwa Waziri wa Wizara ya Fedha alipewa jukumu la kuhakikisha
gharama za kumlipa mkaguzi huyo zinapatikana ndani ya Serikali au BoT
ama pengine popote.
Alifafanua kuwa kati yake yeye na gavana
hakuna aliyekuwa na mamlaka juu ya mwingine na kwamba gavana alikuwa
na wajibu wa kufanya mchakato wa kumtafuta mkaguzi wa dhahabu.
Mramba
alisisitiza kudai kuwa yeye hakuhusika kwenye mchakato huo kwa
kumtafuta wala kumleta hapa nchini wala kumtuma mwakilishi yeyote
kumwakilisha kwenye kamati iliyoteuliwa kufanya mchakato huo bali
alipewa agizo la kumlipa.
“Mimi kama waziri sikuwa na mtu wangu
kwenye ile kamati, lakini Wizara ilituma mwakilishi, ambaye alikuwa
mwanasheria Bethar Soka wakati wa kuhoji kampuni mbili ili wachague na
kwenye kujadili vipengele vya mkataba,”alisema.
Inadaiwa kuwa,
kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, mwaka 2004, jijini Dar es Salaam,
washtakiwa wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na
kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao waliipatia msamaha wa kodi isivyo halali, Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza. |
No comments:
Post a Comment