Sensa ni zoezi la kuhesabu watu wote waliomo nchini,
kujua mgawanyiko wa watu hao katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na
maeneo ya utawala na ukusanyaji wa taarifa nyingine zinazohusiana na watu na
makazi yao.
HISTORIA YA SENSA TANZANIA.
Sensa ya kwanza Tanzania ilifanyika mwaka 1910.
Sensa nne za Mwisho zilifanyika baada ya Uhuru, katika miaka ya 1967, 1978,
1988 na 2002. Kulingana na sensa ya mwisho iliyofanyika mwezi Agosti 2002,
idadi ya watu nchini Tanzania ilikuwa 34,443,603. Sensa ya 2012 itakuwa Sensa ya tano baada ya uhuru.
LENGO KUU LA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012.
- Kwa ujumla, takwimu za sensa ya watu ni za muhimu sana katika kupanga mipango inayohusiana na uchumi, utawala na huduma mbalimbali zinazohitajika katika kuinua hali ya maisha ya watu kitaifa.
- Takwimu zitokanazo na Sensa uchangia katika uboreshaji wa maisha ya Watanzania kwa kutoa Takwimu sahihi na zinazoendana na wakati kwa ajili ya kutunga sera, kupanga mipango ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa program mbalimbali zinazohusiana na maendeleo ya watu. Sense zote ni muhimu lakini Sensa ya mwaka 2012 ina umuhimu wake wa kipekee kwa kuwa itatoa viashiria vingi vitakavyotumika katika kutathimini program za MKUKUTA, MKUZA, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kwa Tanzania Bara na 2020 kwa Tanzania Zanzibar, Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2011/12-2015/16 na Malengo ya Milenia ifikapo 2025. Viashiria hivi muhimu nipamoja na idadi ya watu ki makazi, ukubwa wa nguvu kazi, idadi ya vifo na vifo vinavyotokana na uzazi, wastani wa umri wa kuishi wa Mtanzania, viwango vya uzazi, idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika na idadi ya watoto walioandikishwa shule. Viashiria vingine ni pamoja na idadi ya kaya zinazoshujishughulusha na kilimo, ufugaji na uvuvi.
Madhumuni
ya jumla ya kufanya sensa yamegawanyika katika sehemu kuu mbili;
Sehemu ya kwanza ni ya-kitakwimu na ya pili ni ya-kiutendaji.
2. Madhumuni ya kitakwimu:
Kupima hali ilivyo.
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012
itatoa takwimu kuhusu hali ya uchumi na ustawi wa jamii, kwa kuangalia
mabadiliko yatakayoonekana kwenye sensa hiyo yakilinganishwa na Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2002, kama vile ongezeko na mgawanyiko wa watu ki-umri,
ki-jinsi n.k.
2.1. Kutayarisha mipango ya Maendeleo
Inaeleweka kwamba, Sensa ya Watu hutoa
takwimu zinazowezesha kupima kiwango cha maendeleo kilichofikiwa ili kuandaa
sera na mipango ya maendeleo ya kipindi kinachofuata. Kwa hiyo, sensa ya watu
na makazi ya mwaka 2012 itatoa, pamoja na mambo mengine, takwimu zitakazotumika
katika kupima kiwango cha maendeleo kilichofikiwa na kupanga mipango ya
maendeleo kwa wakati ujao.
2.3. Kuweka misingi itakayosaidia kufanya maamuzi
Idara za serikali na taasisi zake,
mashirika yasiyo ya kiserikali, wafanya biashara, watafiti na watu binafsi,
hutumia takwimu za sensa kama msingi wa kuboresha na kupanua shughuli zao.
2.4. Kupata takwimu kwa maeneo madogo madogo
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012,
itawezesha upatikanaji wa takwimu muhimu kwa maeneo ya vijijini na mijini. Pia,
wilaya zitapata takwimu za watu kuhusu hali zao za kiuchumi na ustawi wa jamii
kwa ajili ya kutayarishia mipango yao ya maendeleo.
2.5. Kutoa mwongozo na msingi wa kufanya utafiti
Matokeo ya sensa, yatatoa takwimu
muhimu ambazo zitatumika katika uchambuzi wa mabadiliko yaliyopo kuhusu
mgawanyiko wa watu ki-umri, mtawanyiko na ongezeko la watu nchini. Hii
itawezesha kuainisha maeneo ambayo yatahitaji kufanyiwa utafiti wa kina ili
kuweza kujua chanzo cha hali iliyopo.
3. Madhumuni ya Kiutendaji:
Uundaji wa sampuli
Kuweka msingi imara wa sampuli
utakaowezesha kuendesha tafiti mbalimbali kati ya sensa moja na nyingine pamoja
na mipango mingine ya ki-Takwimu. Matokeo ya sensa yatasaidia kutoa takwimu za
msingi zitakazosaidia katika kutayarisha msingi wa sampuli utakaotumika
kufanyia tafiti zilizo bora kuhusu mambo ambayo yanatakiwa kutathminiwa mara
kwa mara.
3.1 Kuweka msingi wa kuendesha sensa hapo baadaye
Tanzania imeshafanya sensa nne baada
ya kupata uhuru. Sensa hizi nne na ya mwaka 2012 zitatumika katika kuandaa na
kuboresha sensa za baadaye.
Matumizi ya Takwimu zitokanazo na
Sensa:
Utekelezaji
wa shughuli hii ya kuhesabu watu kitaifa ni jambo la
muhimu sana kwa Taifa. Matokeo ya sensa ya watu, yatatuwezesha kupata picha
kamili juu ya watu waliomo nchini. Kwa maana hiyo, matokeo hayo yatakuwa ni
msingi wa kupanga mipango ya maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii kama vile
elimu, afya n.k
Mifano michache kuhusiana na
suala hili na jinsi Takwimu za Sensa zinavyotumika kutekeleza mambo muhimu ya
kisera ni kama hii ifuatayo:
Kwa mfano, Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii ingependa kupanua huduma za Afya ya Mama na
Mtoto pamoja na kuwaelimisha watu kuhusu utunzaji wa mazingira
katika maeneo ambamo matokeo ya sensa yanaonyesha viwango vya juu vya vifo.
.Takwimu kuhusu umri, zitaonyesha
uwiano kati ya watoto ambao hawajafikia umri wa kwenda kuandikishwa/kuanza
shule na wale ambao wamefikia umri huo; watu wanaojishughulisha na kazi za
uzalishaji mali na wale wanaotoa huduma; vikongwe na wasiojiweza ambao
wanahitaji msaada kutoka serikalini na wadau wengine ili waweze kuishi n.k.
Takwimu hizi vile vile, ni muhimu katika kupanga huduma za akina mama na watoto, shule na walimu, kuboresha huduma za afya, mazingira ya sehemu za kazi pamoja na kutafuta mbinu na kuweka mikakati ya kuinua maisha ya watu kwa ujumla.
Takwimu
za elimu, darasa ambalo mtu anasoma au
alilohitimu, zitaonyesha uwiano wa wanaojua kusoma na wasiojua kusoma, wenye
viwango mbalimbali vya elimu, watoto wanaosoma shule ukilinganishwa na wale
ambao walipaswa kuwa shuleni kutokana na umri wao n.k. Takwimu hizi zitakuwa ni
kigezo muhimu katika kupanga mipango ya elimu ili kuimarisha juhudi za kuondoa
umaskini, ujinga na maradhi.
- Takwimu mbalimbali za kiuchumi, zitatuonyesha uwiano wa watu wanaojishughulisha na kazi za kuzalisha mali pamoja na aina ya kazi zinazofanywa na watu waliomo nchini. Hii itasaidia katika kupanga mipango ya maendeleo inayolenga katika kukuza ujuzi wa wafanyakazi, utoaji wa ajira kwa vijana, uboreshaji wa uzalishaji mali, na upangaji wa maisha bora zaidi kwa watu wote.
- Takwimu kuhusu idadi ya watoto waliozaliwa hai na ambao bado wanaishi, na wale waliofariki, zitaonyesha hali ya uzazi na vifo hapa nchini.
- Takwimu hizi, zitaonyesha jinsi watu wanavyoongezeka na kutuwezesha kufanya makisio ya idadi ya watu katika miaka ijayo kwa nchi nzima, ki-mkoa na ki-wilaya. Hii itatuwezesha kupanga mipango ya maendeleo kwa usahihi.
- Takwimu za sensa zinasaidia katika kutathmini huduma za afya kwa watoto na kina mama. Hii ni muhimu katika kuweka mikakati ya kupambana na vifo vya watoto na vile vinavyosababishwa na matatizo ya uzazi kwa akina mama.
YAFUATAYO NI
MAELEZO YA UFAFANUZI WA
MALENGO YA MILLENIA, MKUKUTA, MKUZA NA DIRA YA MAENDELEO KATIKA KUHAMASISHA
WADAU WA MAKUNDI YA JAMII.
LENGO
Kwa
kuwa Takwimu za Sensa Zitatumika kutathmini malengo ya millennia, ni budi kutoa
ufafanuzi na maana na kuwapa elimu wadau wa Sensa kuhusiana na malengo ya
millennia, Mkakati wa Kupunguza Umasikini na kukuza Uchumi (MKUKUTA) na MKUZA
kwa Tanzania visiwani pamoja na Dira ya Maendeleo
1.
MALENGO YA MILLENIA
Malengo
ya Millenia kama inavyoitwa kwa kiingereza Millenium Development Goals (MDGs)
yalipangwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2000 kule Marekani.
Malengo yanatekelezwa kati ya 2000 – 2015. Malengo haya yako nane nayo ni;
1.1. Kuondoa Umasikini uliokithiri
1.2. Kufikia Elimu ya Msingi kwa
Wote
1.3. Usawa wa Kijinsia na kuwawezesha
wanawake
1.4. Kupunguza Vifo vya watoto
1.5. Kuboresha Afya ya akina mama
wazazi
1.6. Kupambana na Ukimwi na Virusi
vya Ukimwi na Kinga
1.7. Kuhakikisha mazingira endelevu
1.8. Kuendeleza Mshikamano wa
Kimataifa kwa maendeleo
2.
MKUKUTA
MKUKUTA
ni neno maarufu katika jamii ya Tanzania toka ulipozinduliwa mwaka 2005. Kirefu
chake kikiwa ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania. Hivi
sasa tuna Mkukuta II ambao umeboreshwa kutoka katika Mkakati wa kwanza wa
kupunguza umaskini uliozinduliwa Oktoba 2000 na kutekelezwa kuanzia 2005 hadi
2010
Malengo ya Mkukuta yamejikita
katika;
·
Ukuaji wa Uchumi
·
Kupunguza Umasikini wa Kipato
3.
MKUZA
Malengo
ya MKUZA ni;
-Kupunguza
Umasikini wa kipato
-Kuweka
mazingira mazuri kwa uwekezaji
4.
DIRA YA MAENDELEO
Malengo
makuu yamegawanyika katika nguzo nne ambazo ni;
4.1. Nguzo ya kwanza ni kuendeleza
Utulivu wa amani
4.2. Nguzo ya pili ni kutumia fursa
na rasilimali tele za Tanzania (Watu takribani milioni 40, ardhi nzuri ya
kutosha, madini ya kila aina, bahari, maziwa, mito, misitu, wanyama pori, mifugo,
vivutio vya Utalii kemkem n.k) kama mota ya kukuza uchumi
4.3. Nguzo ya tatu ni kutumia nafasi
nzuri sana ya Tanzania kijiografia. Lengo ni kuifanya nchi hii kuwa lango kuu
la biashara na kuhudumia nchi za maziwa makuu na hasa zile zisizokuwa na mlango
bahari (DRC Mashariki, Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Malawi). Kipaumbele ni
kukarabati/kujenga kwanza miundombinu ya kimkakati hasa nishati, bandari, reli,
barabara teule na mkongo wa taifa ili kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi
shindani pamoja na kuongeza ufanisi katika huduma hizo na zile za Mamlaka ya
Mapato.
4.4. Nguzo ya nne ni kukuza matumizi ya TEHAMA (ICT)
kama nyenzo ya kuongeza tija hasa kilimo cha mazao, ufugaji na uvuvi na pia
viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini.
perfect explanation 90%
ReplyDeletenoted perfect explanation
ReplyDeleteNoted
ReplyDelete06:43
ReplyDeletenoted perfect explanation